EN SW

Bayport yakabidhi msaada wa jenereta Halmashauri ya Bumbuli

Na Mwandishi Wetu, Bumbuli

KUTOKANA na kukosa umeme katika ofisi za Halmashauri ya Bumbuli, Taasisi ya kifedha ya Bayport Financial Services, imemkabidhi jenereta Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na kufanikisha maendeleo kwa wakazi na wananchi wa Bumbuli, mkoani Tanga.

Makabidhiano hayo yamefanyika mwishoni mwa wiki iliyopita yakiongozwa na Meneja wa Bayport Kanda ya Kaskazini, Emmanuel Nzutu, Meneja wa Bayport, wilayani Lushoto mkoani Tanga, Consolata Thomas, Mkurugenzi Mtendaji Bumbuli Peter Nyalali, Afisa Utumishi wa Bumbuli Fatma Mrope na baadhi ya watumishi wengine wa halmashauri hiyo.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Meneja wa Bayport Kanda ya Kusini, Nzutu, alisema kwamba taasisi yao imeona ikabidhi msaada wa jenereta kwa mkurugenzi wa Bumbuli ili watumishi kwenye ofisi hiyo watoe huduma bora na kwa wakati ili kuharakisha maendeleo katika serikali ya Hapa Kazi Tu, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dr John Pombe Magufuli.

“Bayport ni taasisi inayotoa huduma za mikopo huku tukifanya kazi kwa karibu na watumishi wengi nchini Tanzania, hivyo baada ya kuona ofisi za Halmashauri Bumbuli hazina umeme na wafanyakazi wanapata tabu, tukaona tuje kuwakomboa kwa kuwapa jenereta.

“Tunaamini sasa wana Bumbuli watahudumiwa vizuri na kwa wakati, maana awali mtu anaweza kukosa huduma pale inapohitaji kifaa kinachoendeshwa na umeme, hivyo Bayport tunaamini tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na kushirikiana na viongozi wote ili kuhakikisha kwamba nchi yetu inasonga mbele,” Alisema.

 

bumbuli 1

Meneja wa Bayport Financial Services, Kanda ya Kaskazini, Emmanuel Nzutu, kulia, akipeana mikono na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli, Peter Nyalali kushoto baada ya kumkabidhi msaada wa jenereta kutoka kwenye taasisi yao ya Bayport kwa ajili ya ofisi ya Halmashauri ya Bumbuli ili iweze kujiendesha vizuri kutokana na ukosefu wa umeme kwenye majengo yao ya ofisi. Nyuma ya Nzutu ni Meneja wa Bayport wilaya ya Lushoto Consolata Thomas, akifuatiwa na Afisa Utumishi wa Bumbuli, Fatma Mrope. Picha na Mpiga picha wetu Bumbuli.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ya Bumbuli, Nyalali, aliwashukuru Bayport Financial Services kwa kuwakomboa baada ya kuwapa msaada wa jenereta litakalowezesha utoaji huduma bora pamoja na ukusanyaji wa mapato na rekodi kwa ofisi muhimu za halmashauri yao.

“Kukosekana umeme kwa ofisi nyeti za halmashauri ni jambo linaloweza kuwafanya watumishi wafanye kazi chini ya kiwango pamoja na kushindwa kukusanya mapato ya serikali kwa wakati kwa sababu kuna vifaa ili vijiendeshe lazima umeme uwepo,” Alisema Mkurugenzi huyo ambaye ameripoti kazini kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa kuongoza halmashauri hiyo.

Afisa Utumishi wa Bumbuli, Fatma Mrope aliwashukuru Bayport huku akisema kupata jenereta kutawafanya watumishi wote wakose visingizio vya umeme hivyo kufanya kazi kwa nguvu zote za kuwatumikia wana Bumbuli na Watanzania kwa ujumla.

“Ofisi za Halmashauri yetu ya Bumbuli ilikuwa na changamoto kubwa ya kukosa umeme, hivyo ingawa tunaendelea na juhudi za kupata umeme kutoka Mamlaka ya Umeme Vijijini (REA), tunafurahia sana msaada huu kutoka kwa watu wa Bayport, maana utakuwa mkombozi kwa kiasi kikubwa mno kwa sababu nikiwa kama Afisa Utumishi naifahamu adha tuliyokuwa tunaipata,” alisema Fatma.

 

bumbuli 4

Meneja wa Bayport Financial Services, Kanda ya Kaskazini, Emmanuel Nzutu, kulia, akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli, Peter Nyalali kushoto baada ya kumkabidhi msaada wa jenereta kutoka kwenye taasisi yao ya Bayport kwa ajili ya ofisi ya Halmashauri ya Bumbuli ili iweze kujiendesha vizuri kutokana na ukosefu wa umeme kwenye majengo yao ya ofisi. Nyuma ya Nzutu ni Meneja wa Bayport wilaya ya Lushoto Consolata Thomas, akifuatiwa na Afisa Utumishi wa Bumbuli, Fatma Mrope. Picha na Mpiga picha wetu Bumbuli.

 

Mbali na kutoa mikopo ya fedha taslimu, Bayport pia inatoa huduma ya mikopo ya viwanja katika maeneo mbalimbali kama vile Kibaha, Chalinze, Bagamoyo, Kigamboni na Kilwa, huku ikifanikiwa kuwa na ofisi katika mikoa yote ya Tanzania Bara na wilaya mbalimbali kwa ajili ya kusogeza huduma zao karibu na wananchi.