EN SW

Mbeya wataka kompyuta za Bayport ziongeze ufanisiwa kazi

DSC_9425

Mratibu wa Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Mercy Mgongolwa, wa pili kutoka kushoto, akimkabidhi kompyuta nane Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Nyasenga Enock kwa ajili ya kuzigawa kwa Halmashauri nne za Mkoa huo wa Mbeya. Wa kwanza kushoto ni Meneja wa Kanda ya Kusini wa Bayport Financial Services, Emmanuel Nzuttu. Wa pili kutoka kulia ni Meneja wa Bayport Mbeya, Mohamed Kisoki akifuatiwa na wakala wake Kurwa Lighton. Picha na Mpiga Picha wetu Mbeya.

Na Mwandishi Wetu,Mbeya

SERIKALI ya Mkoa wa Mbeya, zimewataka watumishi wa umma katika mkoa wao,hususan kupitia ofisi zitakazonufaika na msaada wa kompyuta nane kutoka kwenye taasisi ya kifedha ya Bayport Financial Services, kuongeza ufanisi wa kazi kwa kupitia vitendea kazi hivyo vilivyotolewa.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Mbeya, Nyasenga Enock, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Amos Makalla, kwenye makabidhiano ya kompyuta zilizotolewa na Bayport kwa ajili ya ofisi ya Halmashauri ya Tunduma, Ileje, Mbeya na Rungwe, huku kila ofisi ikipokea kompyuta mbili.

DSC_9426

Majadiliano yakiendelea katika makabidhiano hayo ya kompyuta kutoka Bayport Financial Services mwishoni mwa wiki, mkoani Mbeya.

Akizungumzia hilo, Enock alisema kwamba haitakuwa na maana kama msaada wa kompyuta za Bayport hautaongeza ufanisi kazini na kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kutumia vyema vitendea kazi hivyo vipya vinavyoweza kuleta tija kama kila mtumishi atafanya kazi kwa nguvu zote ili kuwatumikia wananchi.

DSC_9429

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Nyasenga Enock akigawa kompyuta hizo kwa wahusika baada ya kukabidhiwa na Bayport Financial Services.

DSC_9432

Ugawaji wa kompyuta ukiendelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mbeya.

DSC_9434

“Huu ni msaada mkubwa kwa mkoa wetu, hususan wale ambao kwa namna moja ama nyingine watazipokea kompyuta hizi kama ilivyoelekezwa na Ofisi ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ukizingatia kwamba mpango huu ulizinduliwa kwao tangu mwaka jana.

“Nawaomba wale ambao watapokea kompyuta hizi wakafanye kazi kwa nguvu zote tukiamini kuwa wenzetu wa Bayport watakapoamua kufanya utafiti wa vifaa vyao jinsi vilivyotumika, basi kuwe na tija ili waendelee kushirikiana na sisi kwa mambo mengine,” Alisema Enock.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Mratibu wa Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Mercy Mgongolwa, alisema ni furaha yao kuzifikisha kompyuta hizo kwa mkoa Mbeya, ikiwa ni siku chache baada ya kuingia mwaka mpya wa 2017.

“Tunaamini kwa kiasi kikubwa kuwa wenzetu wa Mbeya watazitumia kompyuta tulizo wapa kama sehemu ya kupanua wigo wa kuwatumikia wananchi kwa ajili ya kukuza uchumi wao na Watanzania kwa ujumla kwa namna moja ama nyingine.

“Baada ya kuingia mwaka mpya wa 2017, Mkoa wa Mbea wamekuwa wa kwanza kupokea kompyuta zetu na tunaamini utaratibu huu utaendelea kwa mikoa nyingine kama tulivyojipanga kuhakikisha kwamba tunapunguza changamoto za ukosefu wa kompyuta kwa ofisi za serikali kwa sababu ni jambo la msingi na serikali haiwezi kufanya kila kitu,” alisema Mercy.

Taasisi hiyo inayojihusisha na mikopo kwa watumishi wa umma na wafanyakazi wa kampuni binafsi zilizoidhinishwa, imeamua kusambaza kompyuta 80 kwa ofisi za serikalini mikoani, huku Wizara ya Utumishi Makao Makuu tukiacha kompyuta 125, huku kompyuta zote hizo zikiwa na thamani ya Sh Milioni 500.