EN SW

Kompyuta za Bayport zafikishwa kwa ofisi za Mkoa wa Morogoro Meneja Masoko

0D6A0638-3

Kompyuta za Bayport zafikishwa kwa ofisi za Mkoa wa Morogoro Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo, kushoto, akimkabidhi moja ya kompyuta sita zilizotolewa na Taasisi yao kwa ajili ya kuusaidia Mkoa wa Morogoro katika vifaa vya ofisini ili kurahisisha utendaji kazi. Anayepokea ni Mkuu wa Mkoa Morogoro, Mheshimiwa Dkt Stephen Kebwe, leo mkoani Morogoro. Picha zote na Mpiga Picha Wetu.

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

TAASISI ya Kifedha ya Bayport Financial Services inayojihusisha na mikopo imekabidhi kompyuta sita kwa uongozi wa Mkoa wa Morogoro, kwa kupitia Mkuu wake wa Mkoa, Mheshimiwa Dkt Stephen Kebwe, ili zisaidie utendaji kazi wa watumishi wa umma katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya Mvomero, Manispaa ya Morogoro Mjini pamoja na Morogoro Vijijini.

Ugawaji wa kompyuta hizo ni mwendelezo wa taasisi hiyo kugawa vitendea kazi hivyo baada ya kumkabidhi kompyuta 125 kati ya 205 kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Angellah Kairuki, huku kompyuta zote zikiwa na thamani ya Sh Milioni 500.

0D6A0688

Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo mwenye miwani akifurahia jambo na Mkuu wa Mkoa Morogoro, Mheshimiwa Dkt Stephen Kebwe mwenye suti nyeusi. Kulia kwa Cheyo ni Afisa Tawala wa Mkoa Morogoro, Victor Ndiva na nyuma ni Mercy Mgongolwa, Mratibu wa Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services.

0D6A0690-2Hapa ni Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo mwenye miwani akipiga picha ya furaha na Mkuu wa Mkoa Morogoro, Mheshimiwa Dkt Stephen Kebwe mwenye suti nyeusi. huku akiwa ameshikana mkono na Afisa Tawala wa Mkoa Morogoro, Victor Ndiva. Nyuma kwa Cheyo ni Mercy Mgongolwa, Mratibu wa Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo, alisema kwamba wamejisikia furaha kufikisha vitendea kazi hivyo kwa serikali ya mkoa wa Morogoro.

Alisema taasisi yao inafanya kazi ya utoaji wa mikopo ya fedha taslimu kwa watumishi wa umma na wafanyakazi wa kampuni binafsi zilizoidhinishwa pamoja na ile mikopo ya viwanja kwa Watanzania wote, wakiwamo wajasiriamali.

“Bayport tumejipanga kuhakikisha kwamba tunaboresha utendaji kazi wa watumishi wetu wa umma kwenye ofisi za mikoa na wilaya, hivyo zoezi la kutoa kompyuta litakuwa endelevu kadri tulivyoelekezwa na serikali baada ya kuwapelekea wazo letu la kununua na kusambaza msaada huu kwao.

“Pamoja na kutoa misaada mbalimbali ya kijamii, tunaahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ya kutoa huduma bora ya mikopo kwa watumishi wa umma, ambapo kusudio letu ni kuona wateja wetu wanajikwamua zaidi kwa kuanzisha au kuendeleza biashara zao ili waongeze vyanzo vya kipato na kuacha kutegemea mishahara,” alisema Cheyo.

Naye Mkuu wa Mkoa Morogoro, Dkt Kebwe, aliwashukuru Bayport kwa kujitolea kwenye jamii na kuwakabidhi kompyuta sita ili ziwasaidie mkoani kwao, akiamini kuwa zitachangia utendaji uliotukuka kwa watumishi wa umma.

“Tunawashukuru Bayport kwa kuona tunastahili msaada huu mkubwa kwetu, tukiamini kuwa watumishi wetu watafanya kazi kwa moyo ili kuhakikisha kuwa kila mtu anatimiza wajibu wake ipasavyo kama wote tunavyokusudia,” alisema Dkt Kebwe na kuwasihi Bayport waendelee kujitoa kusaidia matatizo yanayoikabili jamii ya Morogoro na Tanzania kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Kebwe, Mkoa wao upo kwenye mchakato mkubwa wa kupambana na changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuupatia maendeleo Mkoa wao wa Morogoro.

Mikoa na wilaya mbalimbali za Tanzania Bara zinatarajiwa kunufaika na misaada ya kompyuta kwa ofisi za umma kama dira na dhamira ya taasisi ya Bayport kurahisisha utendaji kazi utakaochangia kuleta maendeleo hapa nchini.